Maadhimisho ya Miaka 235 ya Katiba ya 3 Mei nchini Tanzania
30.04.2026
Ubalozi wa Jamhuri ya Poland nchini Tanzania uliadhimisha miaka 235 ya Katiba ya 3 Mei wakati wa hafla iliyofanyika Dar es Salaam, ukiangazia ushirikiano unaoendelea kukua kati ya Poland na Tanzania.
Mnamo tarehe 29 Aprili 2026, Ubalozi wa Jamhuri ya Poland katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliandaa hafla jijini Dar es Salaam kuadhimisha miaka 235 tangu kupitishwa kwa Katiba ya 3 Mei 1791.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye bustani za Ubalozi, Mkuu wa Ofisi Ubalozi, Sergiusz Wolski alikumbusha umuhimu wa kihistoria wa Katiba ya 3 Mei na kusisitiza maendeleo ya mahusiano kati ya Poland na Tanzania. Alieleza kuhusu kuongezeka kwa ushirikiano katika uwekezaji na miundombinu, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa Shirika la KUKE la Poland katika kusaidia mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR, jambo linalochangia kuboresha usafiri na kuimarisha muungano wa kikanda.
Mgeni rasmi, Mheshimiwa Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Poland na Tanzania katika biashara, uwekezaji, kubadilishana maarifa, afya, na mahusiano ya kidiplomasia kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa pande zote mbili.
Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wawakilishi wa serikali ya Tanzania, mabalozi na wanadiplomasia, wafanyabiashara, diaspora ya Poland, pamoja na watanzania waliohitimu vyuo vikuu vya Poland.
Wageni pia walipata fursa ya kuona maonesho ya picha ya “Wanawake Mashuhuri wa Poland”, yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Poland, yakionesha wanawake mashuhuri waliotoa mchango mkubwa katika historia, utamaduni, na maisha ya umma nchini Poland.