Mataifa Mawili. Ubao Mmoja. - Mashindano ya "Urafiki Gambit” ya Chess yafanyika mara ya kwanza jijini Dar es Salaam
07.02.2026
Zaidi ya wachezaji 30 kutoka nchi tano, michezo ya kusisimua, na mshiriki mwenye umri wa miaka 11 - hivi ndivyo yalivyokuwa mashindano ya kwanza ya "Urafiki Gambit” ya Chess yaliyofanyika tarehe 7-8 Februari 2026 jijini Dar es Salaam.
Mashindano ya kwanza ya “Urafiki Gambit” yaliandaliwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Poland nchini Tanzania kwa ushirikiano na Klabu ya Chess ya Chuo Kikuu cha Jordan. Tukio hilo liliwakutanisha wachezaji kutoka Tanzania, Poland, Nigeria, Malawi na India, na kuunda jukwaa la kimataifa la ushindani wa michezo pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mashindano hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Mataifa Mawili. Ubao Mmoja” – ikiashiria urafiki na ushirikiano unaojengwa kupitia michezo. Wachezaji wenye uzoefu pamoja na wapenzi wadogo wa mchezo wa kifalme walikutana katika meza za chess. Mshiriki mdogo zaidi, Chael Nouidui mwenye umri wa miaka 11, alimaliza katika nafasi ya tano kwa jumla kwa kiwango cha kuvutia, akitunukiwa tuzo maalum pamoja na heshima ya “Nyota wa mchezo Inayochipuka.”
Katika hafla ya ufunguzi, Mkuu wa wa Kituo cha Ubalozi (Chargé d’Affaires a.i.) Sergiusz Wolski aliwasilisha shughuli za Ubalozi wa Poland nchini Tanzania pamoja na maeneo ya ushirikiano kati ya Poland na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa mipango ya kitamaduni, kielimu na kimichezo katika kuimarisha mahusiano baina ya nchi mbili. Mkurugenzi wa mashindano, Dkt. Konrad Czernichowski, aliwatambulisha washiriki historia ya mchezo chess nchini Poland na mchango mkubwa wa mabingwa wa Poland katika maendeleo ya mchezo huo katika ulingo wa kimataifa.
Mashindano hayo yalikuwa yamesajiliwa na kupangiwa viwango na FIDE. Mshindi alikuwa Jordan Boksinski, nafasi ya pili ilichukuliwa na Henry Marwa Michael, na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Parsa Naser. Tuzo maalum pia zilitolewa, ikiwemo tuzo ya mchezaji bora wa kike, ambayo ilimwendea Prisha Chheda.
Hafla hiyo ilikusudia si tu kuendeleza mchezo wa chess kama mchezo wenye thamani mkubwa ya kielimu, bali pia kukuza mazungumzo ya tamaduni mbalimbali, kuimarisha mshikamano wa kijamii, na kuhamasisha ushiriki wa vijana. “Urafiki Gambit” imeonesha kuwa ubao wa chess unaweza kuwa jukwaa la kukutana, kushirikiana na kuheshimiana - nje mipaka ya nchi na tamaduni.